Sunday, 3 February 2019

Kwanini Kampuni Inauza Hisa zake

Habari ndugu msomaji wa mtandao huu wa Wekeza Mtanzania, karibu katika mfululizo wa makala za kuhamasisha na kuelimisha kuhusu uwekezaji katika hisa na kuongeza kipato. Asante Mungu kwa siku nyingine, nawakaribisha katika kuongeza maarifa katika kukuza kipato na uhuru wa kifedha.

Kampuni Kuuza hisa 


Karibu katika makala ya leo kuhusu kufahamu sababu za kampuni kuuza hisa zake kwa wakezaji. unaweza kuona kama, makala hii haikugusi moja kwa moja ila nakusihi uendelee kusoma kwa sababu utakachojifunza kitakusaidia katika maisha yako ya kawaida katika biashara zako.

Maisha katika biashara na uwekezaji ni kama ukuaji wa mtoto. Ukuaji wa mtoto una hatua mbalimbali kutoka kuzaliwa kwake na ukuaji wake una changamoto na mifumo ya mabadiliko.
Hata kampuni zinapoanzishwa zinapitia hatua ndogo ndogo hadi kufikia kuitwa kampuni kubwa. Kampuni ina anza na watu wachache ila kila inavyoendelea kukua umiliki na uendeshaji wake unazidi kuongezeka. Na hii ndio njia abayo kampuni ndogo zinapitia hadi kufikia kuwa kampuni kubwa.Kampuni ina machaguo kati ya kukopa au kupata fedha toka kwa mwekezaji inategemea aina ya mradi na kiasi cha fedha ambacho kinahitaji.

Siku za hivi karibuni nilikutana na rafiki yangu ambaye baada ya kuongea mambo mengi toka tulipoacha tukiwa shule alitaka nimuelezee, Kwanini kampuni inauza hisa? Bila kuwa mchonyo nikaona ni vyema nikawashirikisha ndugu wasomaji wa mtandao huu ili na nyinyi mpate kujua machache kuhusu sababu za Kampuni kuuuza hisa zake.

Kampuni inapohitaji kufanya mradi mkubwa ina maamuzi mawili kukopa toka taasisi za fedha kama benki au kupata mtaji toka kwa wawekezaji ambao watakuwa tayari kuweka mtaji wao katika mradi wa kampuni. Na wawekezaji wakitoa pesa katika kampuni husika katika mfumo wa kununua hisa na wao wanakuwa sehemu ya wamiliki wa kampuni.

umuhimu-wa-mwanafunzi-wa-chuo kujijengea nidhamu ya kuweka akiba

Kuna Mfano mdogo ambao utakupa mwanga kwanini Kampuni zinauza hisa katika jamii na wanauzaje?? Mfano huu unahusu mjadiliano ambayo nilifanya na rafiki yangu ambaye alihitaji nimueleze kwanini Kampuni zinauza hisa. Majadiliano yalikuwa hivi

"Nikamwambia kwa mfano Mimi nataka kufungua Duka pale mtaani kwetu"

Akashangaa "eeeh unataka kufungua Duka" Nikamwambia huu  ni mfano tu.

Mfano Nahitaji kufungua duka, mtaji WA bidhaa na gharama za chumba ni Milioni moja,  ila mimi nina laki tisa tu. Nakuomba uniongezee laki moja kwa makubaliano ya kuwa mmiliki wa duka kwa asilimia kumi (10%).

Soma na hi Tafsiri rahisi nini Maana ya Hisa

"Kwa kukubali kutoa shilingi laki moja kwenye mtaji wa duka,  na wewe unakuwa mmiliki wa duka kwa asilimia kumi" Nilimuambia rafiki.

Baada ya mwaka duka likatengeneza faida ya Laki tano, kwa kuwa rafiki yangu wewe ni mmiliki kwa asilimia kumi utapata faida ya shilingi elfu hamsini (Gawio) kama sehemu ya kumi ya faida ya duka.

Baada ya miaka miwili Duka likatengeneza faida nzuri,  tukaona kuna uhitaji wa kufungua Duka jingine lenye mtaji wa milioni moja.

Nikamuuliza Rafiki " Baada ya kufungua Duka la pili,  jumla tuna mtaji wa Shilingi Ngapi?
Akajibu "Milioni mbili"

Kumbuka Rafiki " Mwanzo ulitoa laki moja kama mtaji Na ukawa mmiliki wa Duka kwa asilimia 10%, Na Baada ya miaka miwili duka limekua na kuweza kufungua Duka la pili na mtaji umeongezeka  na kufikia milioni Mbili. Kwa maana hiyo baada ya biashara ya Duka kukua na mtaji wako unakua kutoka laki moja hadi laki Mbili. Hii inaitwa ongezeko la thamani ya umiliki wako (Capital appreciation).

Na ikiwa mtu mwingine akihitaji kukulipa kiasi ambacho unamiliki utakubali Rafiki??  Nikamuuliza
Akajibu Ikiwa mtu atahitaji kuchukua umiliki wangu katika Duka nitamuuzia kwa  laki mbili.

Nikamuuliza kwanini laki mbili Akajibu kwa sababu thamani ya umiliki wangu umeongezeka baada ya duka kutengeneza faida nzuri na kuweza kufungua duka la pili. Jumla ya maduka yote yana mtaji wa milioni mbili na mimi namiliki asilimia kumi ya biashara ya duka (10%).

Na ikiwa watakuja watu watatu wanahitaji uwauzie Akajibu Ikiwa watakuja watu watatu au zaidi wakitaka umiliki wangu nitawauzia kwa laki tatu au zaidi.

Kwanini rafiki yangu yupo tayari kuuza zaidi thamani halisi, kwa sababu anafahamu kuwa umiliki wake una thamani na thamani itaendelea kuongezeka zaidi Baada ya kuona Duka linafanya vizuri na uwezekano wa kufanya vizuri zaidi. Vile vile imekuwa rahisi kwake kuongeza bei za hisa zake za duka baada ya kuona uhitaji umeongezeka. Hapo Rafiki ameweza kuona thamani ya sasa (Current value) na anamatarajio ya thamani kuongezeka zaidi (Expected Value).

Kwa huo mfano rahisi kabisa, unaweza kutambua ni kwanini kampuni zinauza hisa zake. Kampuni inauza hisa kwa sababu;

Wanahitaji mtaji, Mtaji kwa ajili kufanya miradi mikubwa ya kampuni ambayo ina malengo ya kupanua wigo wa biashara, kununua mashine za kisasa au kuongeza ufanisi wa Kampuni ili iweze kutengeneza faida maradufu. Na njia yenye gharama nafuu na kuuza hisa katika jamii na jamii kuwa sehemu ya wamiliki katika hisa.

Kujulika, Kampuni ukishauza hisa zake kwa umma ni njia mojawapo ya kujulikana kwa watu wengi. Kwa sababu ni rahisi kusambaa taarifa zake kwa watu wengi zaidi, ila itakuwa mbaya ikiwa kampuni itafanya vibaya sokoni.

Mwekezaji akinunua hisa atanufaika kwa;

Ongezeko la bei (Capital appreciation) Kama ambavyo tumeona katika mfano hapo juu thamani ya hisa ikiongezeka na mtaji unaongezeka pia. Na hii uchangiwa na kufanya vizuri kwa kampuni na matarajio ya mwekezaji katika kipindi kijacho.

Gawio (Dividend) Jinsi ambavyo kampuni inatengeneza faida ndivyo mwekezaji anavyokuwa na uhakika wa kupata gawio la kutosha.

Asante ndugu msomaji wa mtandao, nakusihi endelea kutembelea mtandao wetu wa Wekeza Mtanzania kwa mafunzo zaidi ili kufikia uhuru wa kifedha kwa kuwekeza katika hisa (Soko la Hisa)

Kwa ushauri au maelezo zaidi tuwasiliane kwa namba 0714 445510 ila unatakiwa kulipia kiasi cha shilingi 10,000/=.

KARIBU SANA

Emmanuel Mahundi
MwandishiWekeza Mtanzania

No comments:

Post a Comment