Monday, 18 February 2019

Mbinu hizi zitakusaidia kuanza Kuweka Akiba Leo

Habari ndugu msomaji wa makala hizi za Wekeza Mtanzania, karibu tena upate kuongeza maarifa sahihi kuhusu uwekezaji katika hisa. Ndugu msomaji umeshaanza kuwekeza katika hisa? Ikiwa umeanza kuwekeza ' Hongera Sana'. Kama bado haujaanza kuwekeza katika hisa nakushauri uanze sasa. Na ikiwa haujui uanzie wapi Nitafute kwa namba hapo chini mwisho wa makala hii nikuelekeze.

Weka akiba


Nimekuwa nikizungumzia kuhusu kuanza kuwekeza, na bado naendelea kukushauri ndugu uanze kuwekeza leo katika kununua hisa za kampuni na uwekezaji katika mifuko ya pamoja. Watu wengi na hata mimi mwenyewe mwanzo nilikuwa nakumbana na changamoto ya kupata pesa ya kuanza kuwekeza. Unaweza kujiuliza nitapata wapi pesa kuanza kuwekeza na ikiwa majukumu ya familia ni mengi au kipato chako ni kidogo. Je upo tayari kushindwa kuanza kuwekeza na kujitengenezea kipato cha baadae kisa tu una majukumu mengi au kipato chako ni kidogo.

Changamoto ya watu wengi kushindwa kujiwekea akiba, imekuwa ikiwakumba watu wengi hasa kwa wale ambao ni waajiriwa katika sekta binafsi na sekta za umma. Baadhi ya sababu ambazo watu wengi wamekutana nazo kuwa na majukumu mengi ya familia kama kulipia watoto ada,chakula,malazi na mahitaji mengi ambayo yanahusu familia pia baadhi wamekuwa na majukumu yanayohusu wazazi, wadogo, ndugu wengine na marafiki.

Changamoto nyingine baadhi yetu tumekuwa tukilalamika kuhusu kupata kipato kidogo katika shughuli zetu za kila siku za ujasiriamali na kwenye ajira rasmi. Waajiriwa wamekuwa wakilalamika kuwa mishahara ni midogo na inawatosha kwa mahitaji ya kula, malazi na mahitaji mengine madogo. Wajasiriamali nao wamekuwa wakilalamika kuwa biashara wanazofanya zimekuwa zikiwatosha kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya nyumbani na hata kuishia kwenye madeni.

Soma na hii Nunua hisa kwenye Kampuni hizi

Kwa changamoto zote hizo ambazo zinawakabili watu ambao wameajiriwa na wale ambao wamejiajiri. Je tuendelee kulalamika kila siku na miaka izidi kwenda na mwisho wa siku uzee utukute katika mahangaiko ya kulalamika kuwa kipato chetu ni kidogo na matumizi ni makubwa.

Mimi nasema hapana kwa sababu hata mimi nilikuwa muhanga wa changamoto hiyo ya kulalamika kuwa kipato ni kidogo. Ila baada ya kupata mbinu chache kuhusu pesa nikatambua kuwa pesa niliyonayo japo ni ndogo inatosha kuweka akiba na kuanza kufanya biashara na kuongeza kipato kingine na pesa nyingine kuwekeza ili niwe na uhuru wa kifedha hapo baadae.

Unaweza kujiuliza naweza nikaanza kuweka akiba ikiwa pesa hii niliyona ni ndogo na pia tayari nina madeni mengi ambayo yananikabili. Katika kitabu cha siku nyingi kinaitwa " The Richest Man in Babylon" na baadhi ya vitabu vingine nilivyosoma viliweza kunipatia mbinu ambazo ziliweza kunisaidia kuanza kuweka akiba  na kisha kuanza kufanya biashara na kuwekeza pia kwa kipato changu kilekile. Vile vile vilinipatia njia za kuweza kuanza kupunguza madeni ambayo nadaiwa na mwisho wa siku nilijikuta sina madeni na akiba yangu ikiendelea kukua.

Soma na Hii Kwanini usinunue hisa zinazouzwa bei ndogo

Nawezaje kuanza kuweka akiba leo

1) MFANYAKAZI (Mwajiriwa)
Sehemu kubwa ya waajiriwa wamekuwa wanategemea kipato toka katika mishahara ambayo wamekuwa wakipata kila mwezi. Mwajiri amekuwa akikulipa wewe mfanyakazi kwa gharama ya muda, nguvu na ujuzi ambao umekuwa ukiutoa katika taasisi au kampuni. Je umewahi kujiuliza kuwa umewahi kujilipa wewe mwenyewe baadaya kupata mshahara kabla hujafanya matumizi yoyote?. Je umekuwa na tabia ya kuandika matumizi yako ya kila mwezi?

Mbinu hizi zitakusaidi kuanza kuweka akiba wewe Mwajiriwa na Mfanyabiashara

a) Ukipata mshahara wako au faida ya biashara yako, kabla ya kufanya matumizi yoyote unatakiwa kujilipa asilimia kumi 10% ya mshahara wako na ikiwa itakuwa ngumu unaweza kuanza na asilimia tano na ikiwa utaanza kuweka asilimia kumi natumai utafurahi pale utakapoona sehemu yako ya kumi ikiongezeka kila mwezi. Angalizo sehemu hii ya kumia ambayo utaweka hautakiwi kuitumia kwa matumizi yoyote na nakushauri ukaifungulia akaunti ya muda maalumu (Fixed account) ambayo hautaruhusiwa kuitoa hadi muda ufike.

Nimezungumzia kuhusu kutoitumia hiyo sehemu ya kumi ya kipato chako kwa jambo lolote, kwa sababu matatizo na dharura zipo kila siku tafuta njia nyingine ya kuzitatua na sio kutumia sehemu hiyo ya kumi.

b) Kuwa akaunti ya dharura
Kama ambaovyo nimesema hapo juu sehemu ya kumi hauruhusiwi kuitumia, ila katika kipato chako kile cha mshahara baada ya kutoa sehemu ya kumi kiasi kilichobaki unatakiwa kutenga sehemu ya pesa na kuweka katika akaunti ya dharura (kama vile ugonjwa, msiba na n.k). Akaunti hii inaweza kuweka kuanzia asilimia ishirini au zaidi kutoka katika kipato chako. Na pesa hii itakusaidia katika kutatua dharua zozote ambazo zitatokea ndani ya mwezi huo, kama kuna msiba wa rafiki, ndugu au umepata na dharura ya ugonjwa pesa hii itasaidia kufanikisha kutatua matatizo.

c) Matumizi yote unayofanya yaandikwe
Uwe  na tabia ya kuandika kabla ya kufanya matumizi na baada ya kufanya matumizi. Unapoenda kufanya matumizi ufanye kulingana na vitu ambavyo uliorodhesha katika karatasi yako. Hata kama kuna kitu utakipenda ukiwa katika matumizi ni muhimu kuzingatia vitu ambavyo ulipanga kununua tu. Hii itakusaidia kudhibiti matumizi yasiyo ya muhimu na nidhamu ya pesa.

d) Pendelea kununua vitu katika maduka ya jumla na uombe punguzo
Katika maduka ya jumla huwa bidhaa zinauzwa bei ya chini ukilinganisha na maduka ya reja reja, kwa hiyo kwa kufanya manunuzi katika maduka ya jumla inakusaidia kupata punguzo la bidhaa na kuokoa pesa. Ukifanya manunuzi pia uwe unaomba punguzo au kununua bidhaa ambazo zipo katika punguzo. Pesa zote ambazo utaokoa kwa kununua katika bei ya chini ni muhimu ukaziweka katika akaunti ya akiba.

e) Punguza au acha baadhi ya tabia au mazoea
Baadhi ya tabia ambazo tunazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuwa na matumizi makubwa toka katika kipato ambacho tunakipata tabia hizo kama ulevi,uvutaji n.k. Ikiwa tutaweza kupunguza au kuacha kabisa basi hiyo pesa inatakiwa iingie katika akaunti ya akiba. Usije ukaacha baadhi ya tabia na hiyo pesa ukaipeleka katika jambo lingine ambalo halina faida yoyote.

f) Nunua nguo kwa ratiba
Uwe na ratiba maalumu ya kununua nguo na sio kila ukiona nguo nzuri ukiwa barabarani unanunua. Ili kulinda pesa zako ni muhimu kuwa na ratiba ya kununua nguo mara moja kwa mwezi au kununua kila baada ya miezi miwili na hii itasaidia kupunguza gharama zisizo za lazima na kukuondoa kwenye madeni.

g) Amua sasa kulipa madeni kwa awamu na kuacha kukopa bila sababu maalumu
Ikiwa una madeni ambayo bado una daiwa ni muhimu kulipa ili uweze kujenga uaminifu kwa watu. Ongea na muhusika ambaye ana kudai na mueleze kuwa una mpango wa kupunguza deni ambalo anakudai kila mwezi. Ila kumbuka kuweka akiba ya asilimia kumi na ndipo ufanye matumizi mengine kama kulipa madeni.

Natumai makala hii imeongeza elimu ya pesa kwako mdau wa mtandao huu, endelea kutembelea mtandao huu na kupata huduma zingine ambazo zitakusaidia katika kufikisha malengo yako ya kukuza kipato.

Kwa ushauri au maelezo zaidi tuwasiliane kwa namba 0714 445510 ila unatakiwa kulipia kiasi cha shilingi 10,000/=.

KARIBU SANA

Emmanuel Mahundi
Mwandishi

Wekeza Mtanzania

2 comments: