Saturday, 7 March 2015

Tafsiri rahisi kuhusu uwekezaji katika Hisa

Najua watu wengi wanahitaji kuwekeza katika Hisa. Ila wengi wao wanashindwa kuelewa maana kamili ya neno "Hisa" na inakuwaje mtu anaitwa mwanahisa wa Kampuni fulani. Ngoja nikupe mfano rahisi ambao utafungua akili yako na kutambua maana halisi ya neno Hisa.Hisa maana yake nini? Ni umiliki wa Kampuni au taasisi. Mfano: Juma anahitaji kufungua duka na ana shilingi 300,000 na biashara inahitaji mtaji wa 400,000. Juma anakuomba uwekeze shilingi 100,000 katika biashara yake ili aweze kufanya biashara kwa kununua hisa na kila Hisa anauza shilingi 5,000. Ukikubali kutoa shilingi 100,000 katika biashara ya Juma unakuwa na Hisa 20. Kwa hiyo kwa kutoa 100,000 katika biashara ya Juma unakuwa mmiliki wa biashara ya Juma kwa Hisa 20 ambayo ni sawa na asilimia 25%.

Ikiwa Biashara ya Juma itapata faida ya Tshs 200,000, atatoa sehemu ya faida kwako ambayo itakuwa 25% ya sehemu ambayo unamiliki, ambayo sawa na shilingi 50,000. Faida hii ambayo atatoa kwako inaitwa gawio (dividend).

"Kumbuka thamani ya duka la Juma ni 400,000 ambayo na wewe unamiliki"

Baada ya muda Biashara ya Juma inaendelea kufanya vizuri na anaongeza bidhaa nyingine katika duka zenye thamani ya shilingi 300,000 na thamani ya duka kuongezeka. Baada ya mwaka mmoja thamani ya duka ni shilingi 700,000.

Na wewe unamiliki asilimia 25% ya biashara kulingana na thamani halisi ya duka. Kwa sasa unamiliki 25% ya thamani ya duka lenye thamani 700,000.

"Kumbuka ulinunua Hisa zenye thamani ya shilingi100,000 kutoka katika biashara ya Juma"

Baada ya mwaka Rafiki yako anakuomba kununua Hisa zako ambazo unamiliki kutoka katika duka la Juma. Kiasi gani anatakiwa kukulipa? Kumbuka unamiliki 25% ya biashara ya Juma.

Asilimia Ishirini na tano ya Tshs 700,000 ni sawa na Tshs 175,000. Waooooh! umepata ongezeko la shilingi 75,000 kwa sababu ulinunu Hisa za Tsh 100,000 hapo mwanzo.  Ongezeko hili linaitwa ongezeko la Bei (Capital appreciation).

Baada ya muda wa miaka miwili Biashara inazidi kukua na kuwa kubwa Rafiki zako wengine wawili wanakuja kukuomba uwauzie Hisa zako kwa sababu wanaimani kuwa Duka la juma linakuwa na anaweza akafungua maduka mengine sehemu nyingine.

Kila mmoja anataka kumiliki Hisa wanashindana wenyewe kwa Bei. Kwa hiyo unaweza kuuza kwa shilingi 200,000 au 300,000 kwa sababu ya ushindani wao katika kununu Hisa zako. Kwa hiyo tunaona hapo Bei ya Hisa inategemea na vitu viwili thamani halisi ya biashara Juma au thamani inayotegemewa toka katika biashara ya Juma ( wanategemea kuwa atafungua matawi sehemu nyingine).

Kwa hiyo Mfano huu rahisi ndivyo Uwekezaji Katika Hisa unavyofanyika katika soko la Hisa la Dar es salaam (DSE). Nakushauri anza sasa kuwekeza kwenye Hisa kwa kutengeneza utaratibu wa Kununua Hisa kila mwezi au kwa kila kipindi fulani ndani ya mwaka na kuwa na malengo ya kuwekeza kwa muda mrefu.

"Wekeza Inalipa"

Kwa ushauri/maoni mawasiliano
emmmanuelmahundi@gmail.com
0714 445510Wekeza Mtanzania

No comments:

Post a Comment